LOWASA KAJIVUA NGUO ASEMA NAPE.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), jana kimetoa tamko rasmi juu ya uamuzi mgumu uliochukuliwa na Waziri Mkuu wa zamani, Bw. Edward Lowassa ambaye hivi karibuni alikihama chama hicho na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Bw. Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha aliyemaliza muda wake kwa tiketi ya CCM, alichukua uamuzi huo akidai ameamua kuondoka CCM baada ya chama hicho kutomtendea haki katika mchakato wa kumpata mgombea urais, Mjini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Bw. Nape Nnauye, alisema chama
hicho hakibabaishwi na Bw. Lowassa kuhamia CHADEMA pamoja na wenzake  wao si wa kwanza au wa mwisho kuondoka CCM.

Alisema wapo wanachama wengi waliohama kutoka chama kimoja cha siasa kwenda vingine hivyo kuhama kwao si jambo la ajabu ambapo CCM kunaamini uamuzi walioufanya ni wa kawaida ndio maana waliupuuzia na kufanya shughuli nyingine za chama.

"Kuhama kwao CCM si jambo geni ndio maana hatukuona umuhimu wa kuhangaika nao....mwaka huu waelewe kuwa, CCM kitaibuka na ushindi wa kishindo na tutawagalagaza.

"Lowassa na wenzake wamejivua nguo mbele ya Watanzania ambao mwisho wa siku, watawaadhibu kwani wananchi wanataka viongozi
wanaoshughulika nao; si kufanya mambo yao wenyewe," alisema.

Aliongeza kuwa, kuna watu wanaohamia kwenye vyama vya siasa ili kutaka uongozi na wengine wanataka kwenda kuongoza watu ambapo yule
anayetaka kwenda kuongoza watu ni mvumilivu, mtulivu na anafuata taratibu, wengine wanataka uongozi wautumie kwa masilahi binafsi na wakiukosa huonesha mapungufu yao waziwazi.

Alisema kipindi cha nyuma, viongozi waliohama CCM walikuwa wakikifurahia chama hicho kwa sababu walipata fursa na walipoikosa katika jambo walilokuwa wanalitaka wanakiona chama hakifai.

Bw. Nnauye alisema Watanzania wanapaswa kutulia kwani chama chao CCM, mwaka huu kitapata ushindi mkubwa kutokana na operesheni iliyofanywa na Katibu Mkuu, Bw. Abdulrahman Kinana aliyezunguka mikoa yote nchini ili kukijenga chama hicho.

Aliongeza kuwa, inashangaza kuona makada hao (Lowassa na wenzake), wanatoa maneno ya kukikashifu chama baada ya kuondoka na kuhoji  mbona walipokuwa ndani ya CCM hawakusema kitu.

"Mwaka 1995, Augustino Mrema aliondoka CCM na maneno mengi kama akina Lowassa na wenzake...hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema mwacheni na kilichomkuta ninyi waandishi wa habari ni mashahidi.

"Tatizo lililopo, baadhi ya vyama vya siasa vinahangaika na oili chafu ambazo zitasababisha mashine zao kunoki na kushindwa vibaya, CCM hakina muda wa kuiba kura, tunajiamini na tukishindwa huwa tunakubali matokeo, katika maeneo mengi tumeshindwa na kukubali matokeo kwa sababu tunaijua demokrasia," alisema.

Alisema siasa ni sawa na hesabu ambapo CCM kimekaa mezani na kuona ushindi upo tena wa kishindo.

Kura za maoni CCM

Akizungumzia mchakato wa kura za maoni ya ubunge na udiwani kugubikwa na vitendo vya rushwa, alisema takwimu walizonazo ni kwamba, mwaka huu malalamiko yamepungua ukilinganisha na miaka iliyopita ambayo kulikuwa na vurugu kubwa.

Alisema hali hiyo imetokana na kuboresha kwa mfumo wa kuwapata wagombea kupitia kura za maoni lakini mwaka huu, vurugu zimetokea katika maeneo machache na zinatafutiwa ufumbuzi kwa njia ya demokrasia kama iliyotumika kuwapata wagombea.

"CCM ni waumini wa demokrasia tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo vinatoa wagombea wake mifukoni...matukio ya vurugu katika mchakato wa kura za maoni yanakuzwa na vyombo vya habari.

"Tukibaini kulikuwa na vitendo vya rushwa katika mchakato huu, chama kitachukua hatua ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wahusika kwani sisi tunatumia zaidi kanuni na taratibu," alisema.

Bw. Nnauye aliongeza kuwa, kushinda katika kura za maoni si uteuzi bali Kamati za chama zitakaa na kuujadili mchakato huo katika majimbo yote na ikibainika taratibu zilivunjwa, watafuata kanuni na taratibu
ikiwa ni pamoja na kubadilisha matokeo yote.

Dkt. Mahanga kuhamia CHADEMA

Katika hatua nyingine, Bw. Nnauye alisema kitendo cha aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga ambaye pia ni Mbunge wa Segerea ambaye amemaliza muda wake kwa tiketi ya CCM kuhamia CHADEMA, si kitu cha kushangaza kwani alishafanya uamuzi wa kuhama ila alikuwa anatafuta sababau za kuondoka kwake.

Alisema Dkt. Mahanga anafahamu taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa kama anaona hajatendewa haki katika mchakato wa kura za maoni kwenye Jimbo la Segerea baada ya kuangushwa na mpinzani wake ila wanashangaa kuona anapiga kelele.

"Sisi tunajua Dkt. Mahanga amemfuata rafiki yake (Lowassa), tunasema aende tu, tunamtakia safari njema," alisema.

Kukamatwa na TAKUKURU

Akizungumzia madai ya kukamatwa kwake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), katika Jimbo la Mtama, mkoani Lindi, ambako alishinda kura za maoni ya ubunge, Bw. Nnauye alisema taarifa za kukamatwa kwake zimeenezwa, kutangazwa vibaya.

Alisema kinachosemwa kilikuwa na lengo la kumdhoofisha kisiasa ila wapinzani wake hawajafanikiwa kwani ameshinda kwa kishindo katika mchakato wa kura za maoni jimboni humo.

Aliongeza kuwa, siku ya tukio alikuwa akitoka benki kuchukua pesa za kuwalipa mawakala wake akazuiliwa na Maofisa wa TAKUKURU ambao walikuwa wakiongozwa na Kamanda wao wa Mkoa ambapo alihojiwa kwa dakika 20 na si kwa saa tano kama ilivyoripotiwa.

"Ni kweli Maofisa wa TAKUKURU walinihoji, huo ni utaratibu wa kawaida hasa kipindi hiki ambacho taasisi kama hii imekuwa ikidili na wanasiasa...mimi nisingeweza kukataa kwani wale ni Maofisa
wa Serikali, juhudi za kunichafua zilifanywa na mafisadi," alisema.

LOWASA KAJIVUA NGUO ASEMA NAPE. LOWASA KAJIVUA NGUO ASEMA NAPE. Reviewed by WANGOFIRA on 07:17:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.