LIGI KUU ENGLAND: Ukuta Arsenal na safari ndefu ya ubingwa



London, England.
Wiki moja tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu England 2015/16, tayari mashabiki wa klabu ya Arsenal wameanza kuingiwa hofu.
Hofu yao imeondoa matumaini makubwa waliyokuwa nayo kwa klabu yao kuwa inaweza kumaliza zaidi ya miaka kumi bila ya taji la ubingwa wa Ligi Kuu.
Hata hivyo, matokeo mabaya dhidi ya West Ham katika mchezo wa ufunguzi wa msimu Jumapili iliyopita ilipofungwa mabao 2-0 yamerejesha wasiwasi huo wa mashabiki hao.
Ubingwa wa Kombe la FA msimu uliopita, mataji madogo ya mechi za maandalizi ya msimu mpya pamoja na Ngao ya Jamii yalianza kuwatia hamasa mashabiki hao wakidhani msimu huu utakuwa wa kicheko kwao.
Baadhi ya mashabiki au hata wachambuzi wa masuala ya soka wanaiangalia safu ya ulinzi ya kikosi cha Arsenal kwa jicho la hofu, wakijiuliza, je, inao uwezo wa kuhimili vishindo na hatimaye Mei 2016 kuibuka bingwa?
Furaha waliyokuwa nayo mashabiki baada ya kusajiliwa kwa kipa Petr Cech kwa Pauni 11 milioni akitokea Chelsea ilizimika ghafla baada ya makosa yake mawili na safu yake ya ulinzi kuiacha West Ham ikiondoka Emirates na ushindi na pointi tatu.
Wasiwasi mwingi wa mashabiki ni jinsi safu ya ulinzi ya klabu hiyo inavyocheza. Wapo wale wanaoiona safu hiyo kuwa dhaifu, haina watu kama John Terry aliyemfichia makosa Cech akiwa Chelsea na kucheza vyema naye kwa miaka 11 ya mafanikio akiwa Stamford Bridge.
Ukuta wa Arsenal, unaonekana mwepesi, dhaifu licha ya kuwa na wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu katika soka ya England.
Swali linaloulizwa ni je, safu hiyo ni imara kwa kiasi cha kutosha, inao uzoefu wa kutosha? Je, walinzi wa Arsenal wanajitambua wanapocheza?
Uzoefu wa msimu uliopita
Ni ukuta uliocheza vyema msimu uliopita. Ni mabingwa, Chelsea  walioruhusu mabao 32 na  Southampton, mabao 33 waliokuwa na idadi ndogo ya mabao ya kufungwa kuliko Arsenal  iliyoruhusu mabao 36.
Msimu huo, Arsenal ilicheza mechi tatu bila kuruhusu bao, ilitwaa Kombe la FA  dhidi ya Aston Villa, ambayo washambuliaji wake walishindwa kupenya ukuta wake kwenye uwanja wa Wembley.
Kwa maana hiyo, kuwapo kwa Cech ambaye hakuna shaka ni kipa mwenye kiwango cha kimataifa, kunaipa Arsenal nafasi ya kusaka ubingwa,  2015/16.
Kama ambavyo imetokea kwa vijana hao wa Arsene Wenger katika miaka iliyopita, safu ya ulinzi ya klabu hiyo lazima ijiangalie upya, hasa kwa makosa ambayo imekuwa ikiyafanya mara kwa mara.
Ni wapi penye upungufu?
Mwaka mmoja uliopita, kinda Hector Bellerin asingefikiria kuwamo kwenye kikosi cha kwanza cha  Arsenal, lakini anauanza msimu  akiwa na rekodi ya mechi 24 kwenye kikosi cha kwanza, ingawa baadhi ya mechi zilikuwa  za Kombe la FA na lile la Ligi (Capital One).
Hata hivyo, beki huyo chipukizi raia wa Hispania amezoea haraka maisha na mikiki ya soka England, kiasi cha kuwa matumaini ya klabu hiyo msimu huu.
Akiwa na miaka 20, Bellerini anatoa nafasi ya kuwa chaguo la kwanza kwa kocha wake, akiwa tegemeo kwenye kusaidia mashambulizi akitokea upande wa kulia, akionyesha kuwa beki aliyekamilika. Ana nafasi ya kuwa chaguo la kwanza.
Aliziba pengo la Mathieu Debuchy na Calum Chambers, ambao awali walicheza kwenye nafasi hiyo, ingawa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa benchi kwenye fainali ya Kombe la FA.
Ni nini nafasi ya wawili hao?
Debuchy, mwenye miaka 29 hakuwa na bahati kutokana na kuumia kwanza enka wakati wa mechi dhidi ya Manchester City, Septemba, kisha maumivu ya bega dhidi ya  Stoke City mwezi Januari, matukio yaliyotatiza nafasi yake katika msimu wake wa kwanza akiwa kwenye klabu hiyo. Nafasi yake ilizibwa kwanza na Chambers, kisha Bellerin, mabeki ambao wana miaka 20.
Pengine akiwaona makinda hao wawili waking’ara, hakuna shaka beki huyo wa zamani wa Newcastle ana hofu. Anajiuliza, iko wapi nafasi yake ya kucheza kwenye kikosi cha Wenger msimu huu?
Naye  Chambers, ambaye ana miezi miwili ya kuzaliwa zaidi ya Bellerin  ameshuhudia maendeleo ya mpinzani wake sehemu ya pili ya msimu uliopita. Lakini, akiwa bado na miaka 20, ana nafasi kubwa ya kurekebisha makosa na kurejea kikosi cha kwanza na kupata mafanikio makubwa zaidi miezi michache ijayo.
Beki ya kati Arsenal
Hilo ni eneo ambalo linavuta hisia za mashabiki wengi wa klabu hiyo. Hapo unakutana naye, Laurent Koscielny,  ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Arsenal.
Amekuwa na miaka ya mafanikio akiwa Emirates kwa miaka minne ambako sehemu ya beki ya kati ya klabu hiyo imeimarika licha ya beki huyo kuwasili England akiwa hajulikani.
Umuhimu wake unaonekana dhahiri kwani alipokosekana kati ya Oktoba na Novemba, pia Desemba mwaka jana, uwezo wa klabu yake kuhimili ushindani ulipungua, ambako ilipoteza mechi tano dhidi ya Hull, Swansea, ManUnited, Stoke na Liverpool. Katika mechi hizo, Arsenal ilifungwa mabao   11, idadi ambayo ingekuwa pungufu kama angekuwapo.
Baadhi ya mabao yalitokana na kukosekana kwake, kukosa ushirikiano au udhaifu wa mwenzake, Per Mertesacker. Beki wa zamani wa Liverpool  na England, Jamie Carragher alieleza katika uchambuzi wake kwenye Sky Sports 1 (ambao ulipatikana pia kwenye gazeti la Daily Mail) kwamba beki huyo Mjerumani alikuwa chanzo cha matokeo mabaya yakiwamo ya mabao 3-2 dhidi ya Stoke mwezi Desemba.
Alieleza kuwa mchezo huo ulionyesha udhaifu kwa beki huyo wa kikosi cha Ujerumani kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka jana nhini Brazil, ambaye alionyesha kuwa bila msaada wa Koscielny hawezi kitu, si msaada kwa Arsenal.
Mertesacker, beki mrefu amekuwa akikosolewa kwa kwa kukosa kasi. Mara nyingi, amekuwa chanzo cha mabao ambayo klabu yake imefungwa, ingawa alifuta makosa yake kwa kumdhibiti aliyekuwa mshambuliaji wa Aston Villa, Christian Benteke kwenye fainali ya Kombe la FA.
Akiwa na umri wa miaka 30, beki huyo anaonyesha kuwa na miaka michache  ya kuendelea kuiwakilisha klabu hiyo. Alionyesha kuimarika kiasi sehemu ya mwisho ya msimu uliopita.
Kama alivyoonyesha kwenye mechi za mwisho wa msimu, Mertsesacker  alinufaika na usajili wa mwezi Januari wa beki Mbrazili Gabriel kama kichocheo cha kuzidi kubakia kwenye nafasi yake. Kama motisha, beki huyo wa zamani wa Villarreal ameonyesha kuwa anayehitajika.
Akiwa na umri wa miaka 24, bado Gabriel ana nafasi ya kuisaidia Arsenal akiwa tayari ameingia kwenye mipango ya Wenger.
Kwa sifa pekee, unaweza kudhani kwamba Gabriel angecheza zaidi badala ya Mertesacker au Koscielny. Lakini  Arsenal ina mechi nyingi kwa msimu ambazo zitampa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, pia anaendelea kuzoea maisha ikiwamo ya kumudu lugha ya Kiingereza ambayo ilikuwa shida kwake kwa mawasiliano.
Kwa sasa, Arsenal lazima iangalie namna ya kumtumia Gabriel zaidi kwa lengo la kumpa uzoefu akiwa tayari ameonyesha kiwango kizuri.
Beki ya kushoto
Upande huo unao, Kieran Gibbs na Nacho Monreal, eneo ambalo wakati mwingine linaumiza vichwa vya makocha wa klabu hiyo.
Msimu uliopita,  safu hiyo ya kushoto imekuwa kama ugonjwa wa moyo kwa  Arsenal, ambako  Gibbs  ambako mwaka  2014 yeye na Monreal wanauanza msimu  huu wa 2015 wakiwa dhaifu.
Monreal aliyecheza badala ya Gibbs kwa msimu uliopita alionyesha kuwa imara akirejesha uhai kwa Arsenal. Mwezi  Juni, alionyesha dhamira ya  kusaini mkataba mpya na klabu hiyo akiwa tayari kuonyesha makali yake.
Hata hivyo, swali linaloulizwa ni ubora wake kama beki anayeweza kuanza kikosi cha kwanza akiwa beki wa kushoto kila mara? Pia, Gibbs ataendelea kuwa fiti na kuisaidia Arsenal msimu huu?
Msimu umeanza, tayari udhaifu umeonekana katika mechi dhidi ya West Ham, lakini bado wachezaji hao wanatakiwa kubadilika kumwonyesha kocha wao, Wenger kwamba wapo tayari kwa kazi. Hata hivyo, kocha huyo lazima apate mbadala wa Monreal, Gibbs, ingawa wakati mwingine amekuwa akimchezesha Francis Coquelin.
Mfaransa Coquelin, ambaye ni beki anacheza pia kama kiungo, anaweza kuwa dawa kwa safu ya ulinzi ya Arsenal ambayo imekuwa na tatizo kwenye ulinzi.
Hata hivyo, upungufu mkubwa kwa mabeki wa Arsenal ni kucheza bila ngao mbele yao kwa miaka mingi, hasa kwa beki anayeweza kukimbia, kukaba na kutoa pasi.
Kwa kumchezesha Coquelin katika kikosi cha kwanza tangu mwanzo wa msimu ni kitu ambacho   Wenger atakuwa kama kocha amewapa mabeki wake ulinzi unaohitajika. Ulinzi huo, unaweza kuwasaidia kufanya vizuri msimu huu na ikiwezekana kusaka taji.
Hakuna shaka, kuna na safu imara ya ulinzi kuweza kukabili changamoto zote za msimu inategemea mambo mengi kwani klabu kama  Liverpool msimu wa 2013/14 ilifungwa mabao 50 , Chelsea msimu uliopita ilianza msimu  ikipewa nafasi ya kuibuka bingwa, lakini safu imara ya ulinzi ilisaidia kuipa matokeo mazuri.
Kwa upande wake, Arsenal haina shaka inao walinzi wanaoweza kuibeba na kupigania ubingwa, ambao lazima wawasaidier Cech  na Coquelin  kutoa matunda bora. Ni suala la muda na kusubiri kuona.
LIGI KUU ENGLAND: Ukuta Arsenal na safari ndefu ya ubingwa LIGI KUU ENGLAND: Ukuta Arsenal na safari ndefu ya ubingwa Reviewed by WANGOFIRA on 05:42:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.