MATOKEO UBUNGE CCM, MAPINDUZI YAENDELEA



MATOKEO ya kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kwa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini, yameendelea kutangazwa.

DODOMA
Kibakwe-Mpwapwa
Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe, aliyemaliza muda wake, Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, George Simbachawene amefanikiwa kutetea nafasi yake baada ya kuibuka na ushindi wa kura 18,159.

Katika Jimbo la Mpwapwa, mbunge wa zamani jimboni humo Bw.George Lubeleje, ameweza kuwashinda wagombea wenzake tisa  akiwemo mbunge aliyekuwa madarakani, Bw. Gregory Teu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi jimboni humo, Bw. Edward Mbogo alisema Bw. Lubeleje alipata kura 6,700.

MTWARA
Nanyumbu-Mtwara
Aliyeshinda kwenye Jimbo la Nanyumbu, mkoani Mtwara ni Bw. Wiliam Dua ambaye alipata kura 6,168, kwa mujibu wa Katibu wa CCM wilayani humo, Bw. Juma Nachembe akimshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dustan Mkapa.

Katika Wilaya ya Masasi, Katibu wa CCM wilayani humo, Mwanamasudi Paz, alimtangaza Mariam Kasembe kuwa mshindi wa kura za maoni Jimbo jipya la Ndanda baada ya kupata kura 5,453.

Jimbo la Lulindi, mbunge aliyemaliza muda wake, Jerome Bwanawesi alichaguliwa tena kwa kura 11,745 ambapo kwenye Jimbo la Masasi, Rashid Chuachua aliongoza kwa kura 2,412.

DAR ES SALAAM
Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Bw. Ernest Charles, alisema mshindi katika Jimbo la Segerea ni Bonna Kaluwa ambaye alipata kura 6,665,
Scholastika Kevela (6,155), Dkt. Makongoro Mahanga (2,381).

Akizungumzia kuhama kwa Dkt. Makongoro kutoka CCM kwenda CHADEMA, alisema chama hicho wilaya hakina taarifa za kuondoka kwake wala malalamiko aliyotoa kuhusu shahada feki.


SIMIYU NGUMI TUPU
Matokeo ya kura za maoni kwa watia nia ya ubunge Jimbo la Busega, mkoani Simiyu, yamezua kizaazaa na kusababisha ngumi kupigwa katika kikao kilichokuwa kikihakiki kura za wagombea ikidaiwa mgombea mmoja kaongezewa kura.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya wilayani humo, Mwenyekiti wa Kata ya Lamadi, Joel Ludala, alisema hawakubaliani na uchakachuaji wa matokeo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Paul Mzindakaya, alidai walikubaliana kwenda katika vituo vyenye utata, lakini kabla hawajaenda kukatokea vurugu na karatasi za matokeo kuporwa.

Kutokana na uporaji huo, hadi sasa hakuna matokeo yaliyotangazwa kwa washindani wawili kati ya Dkt. Raphael Chegeni na Dkt. Titus Kamani.

Katibu wa CCM mkoani humo, Hilda Kapaya, alisema wagombea wamegawanyika kutokana na matokeo waliyopewa na mawakala
kutofautiana kwenye vikao, hivyo wanasubiri uamuzi kutoka Makao Makuu ya CCM baada ya karatasi za kura kuporwa na mmoja wa wagombea.

ZANZIBAR
Katika hali isiyo ya kawaida, matokeo ya kura za maoni katika majimbo tisa ya Mkoa wa Kaskazini, Zanzibar, yamekwama kutangaza washindi baada ya wagombea kurushiana tuhuma za kupandikizwa kura bandia katika Kituo cha Mahonda.

Utata huo umejitokeza baada ya wagombea sita nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mahonda, kumtuhumu Msimamizi wa Tawi la Mahonda wakidai aliingia na karatasi za wapigakura pamoja na orodha za wanachama ili kumbeba mgombea mmoja wa nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Katibu CCM mkoani humo, Bw. Mula Othman Zubeir, alisema wagombea sita wamelazimika kupewa onyo kwa kuibua tuhuma za uongo hivyo kuathiri uchaguzi wa jimbo hilo.

Aliwataja wagombea hao kuwa ni Bw. Mwinyi Jamali, Bw. Haji Machano, Bi Bahati Ali Abeid, Bw. Omar Bakari, Bw. Almas Muhina Almas na Bw. Ame Khamis ambao wanadaiwa kumdhalilisha mgombea mwenzao Bi. Kidawa Himid Saleh na uchaguzi umelazimika kurudiwa jana.

Katika Jimbo la Kijini, kulitokea matatizo ya karatasi za wapigakura kupelekwa kinyume na idadi ya wapigakura 12,000 badala yake zilipelekwa nakala 3,700 za uwakilishi na ubunge 3,700 ubunge.

Mkoa wa Kaskazini Unguja una majimbo tisa ambayo ni Tumbatu, Nungwi, Chaani, Mkwajuni, Bumbwini, Kiwengwa, Mahonda, Kijini na Donge.

UDIWANI-DAR ES SALAAM

Katika kata ya Makuburi, Jimbo la Ubungo, Wilaya ya Kinondoni, Dar
es Salaam, mshindi wa kura za maoni kwa tiketi ya CCM ni Olivery Shirima ambaye alipata kura 1,401.

Akizungumza na gazeti hili, Shirima alisema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkali lakini wana CCM kwa utashi wao, wamemwona yeye kuwa ndiye anayefaa kuwa diwani wa kata hiyo.

Mshindi wa nafasi ya udiwani katika kwa tiketi ya CCM katika Kata ya Kunduchi, Wilaya ya kinondoni ni Bw. Michael Urio, ambaye alipata kura 1,552.

Alisema uchaguzi huo ulikuwa na changamoto nyingi ingawa hazikuweza  kuvuruga uchaguzi likiwemo suala la rushwa kwa baadhi ya wagombea kuwashawishi wanachama ili waweze kuwachagua.


 

MATOKEO UBUNGE CCM, MAPINDUZI YAENDELEA  MATOKEO UBUNGE CCM, MAPINDUZI YAENDELEA Reviewed by WANGOFIRA on 07:10:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.